Breaking


Jumatano, 20 Mei 2026

TANZANIA INAFANYA MAANDALIZI UPANUZI MIJI PEMBEZONI KUKABILIANA NA UKUAJI WA MIJI-PROF SHEMDOE


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele katika maandalizi ya upanuzi wa haraka wa miji pembezoni ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na fursa za ukuaji wa miji na majiji nchini Tanzania.

Prof. Shemdoe ameelezea hatua hiyo ya Serikali aliposhiriki mdahalo nchini Azerbaijan ambao ni sehemu ya mkutano mkubwa wa kidunia wa masuala ya Miji (World Urban Forum), baada ya kuulizwa ni hatua zipi zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kujiandaa kwa upanuzi wa haraka wa miji pembezoni ili kukabiliana na athari za kukua kwa miji na majiji ikiwepo changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira.

Amefafanua kuwa, hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita kufanya maandalizi ya mapema ya upanuzi wa miji na majiji pembezoni ni muhimu kwani lango kuu la jiji la Dar es Salaam, pamoja na ya majiji ya Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha yanakua kwa kasi isiyokuwa ya kawaida.

Upanuzi wa miji na majiji pembezoni ukitokea bila kuwepo na mipango ya mapema unasababisha ukosefu wa ajira na makazi yasiyo rasmi ambayo hayana maji safi, umeme wa uhakika, na usafi wa mazingira unaostahili, hivyo kurekebisha miundombinu katika maeneo hayo kunaigharimu zaidi Serikali wakati maandalizi yangefanywa mapema gharama za ujenzi wa miundombinu zingekuwa nafuu.

Hakuna maoni: