Breaking


Jumamosi, 23 Mei 2026

TANZANIA NA BRAZIL ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO ZAIDI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Brazil zimeahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya mataifa hayo mawili kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.

Azma hiyo imebainishwa kufuatia mazungumzo kati ya Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, na Balozi wa Brazil nchini, Mhe. Gustavo Martins Nogueira, yaliyofanyika Mei 26, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kujadili utekelezaji wa masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano wa Mashauriano ya Kisiasa uliofanyika mwezi Aprili mjini Brasília, Brazil, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, elimu, mifugo, utalii, biashara na uwekezaji.

Bi. Maduhu ameishukuru Serikali ya Brazil kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Vilevile, Bi. Maduhu amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kufungua fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Balozi Nogueira amesema Brazil itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo ya kijamii, ikiwemo programu za kupunguza umaskini, lishe mashuleni na utoaji wa huduma za kijamii.

Aidha, Balozi Nogueira amesema sekta ya mifugo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa ya ushirikiano, na kwamba Brazil itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuboresha ubora wa mifugo kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza tija, thamani na ushindani wa bidhaa za mifugo katika soko la kimataifa.

Hakuna maoni: