Serikali za Tanzania na Kenya zimeingia katika hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda baada ya kusaini makubaliano muhimu katika sekta ya nishati, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme na kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, pamoja na Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Opiyo Wandayi. Lengo kuu la makubaliano hayo ni kuanza rasmi biashara ya umeme kati ya Tanzania na Kenya, pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa.
Hafla ya utiaji saini imefanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa.
FAIDA ZA USHIRIKIANO HUUMakubaliano haya yanatarajiwa kuleta manufaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki, kupanua biashara ya umeme, kuvutia uwekezaji katika miundombinu ya nishati, pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi.
Aidha, mradi wa bomba la gesi unatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuboresha upatikanaji wa nishati safi kwa matumizi ya viwandani na majumbani.
HATUA MUHIMU KWA MAENDELEO YA KIKANDA
Ushirikiano huu ni sehemu ya jitihada za nchi za Afrika Mashariki kuunganisha rasilimali na miundombinu ya nishati ili kufikia maendeleo endelevu. Serikali zote mbili zimeeleza dhamira ya kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni