Kauli hiyo imetolewa Mei 20, 2026 jijini Nairobi nchini Kenya na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ambaye pia ni Rais wa Baraza la 14 la Uongozi wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka, wakati akifungua kikao cha baraza hilo.
Katika hotuba yake, Dkt. Kijaji amesema ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika ni muhimu katika kupambana na mitandao ya kimataifa inayojihusisha na biashara haramu ya wanyamapori, ujangili pamoja na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
Amesema Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kuimarisha uhifadhi wa maliasili kupitia hatua mbalimbali zilizotekelezwa ndani ya mwaka mmoja tangu ichukue uongozi wa Baraza hilo mjini Arusha.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, Serikali imeongeza juhudi katika uhifadhi shirikishi kwa kushirikiana na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinaendelea kulindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amesema wanyamapori na misitu si mali ya taifa moja pekee, bali ni urithi wa dunia unaohitaji kulindwa kwa ushirikiano wa pamoja ili kuzuia uharibifu unaoweza kuathiri mazingira na uchumi wa mataifa mbalimbali.
“Mapambano dhidi ya ujangili hayawezi kufanikiwa kwa matamko ya kisiasa pekee. Yanahitaji utekelezaji wa vitendo, ubunifu, uwekezaji na mikakati yenye matokeo chanya,” amesema Dkt. Kijaji.
Kikao hicho kimewakutanisha nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka zikiwemo Tanzania, Kenya, Zambia, Congo Brazzaville na Liberia, kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kudhibiti makosa ya wanyamapori na misitu.
Mkutano huo pia umetokana na maazimio yaliyofikiwa katika kikao cha 14 cha Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka kilichofanyika Mei 2025 jijini Arusha, Tanzania.
Sambamba na kikao hicho, Dkt. Kijaji alizindua rasmi Mpango Mkakati wa Sekretarieti ya Mkataba wa Lusaka wa mwaka 2025 hadi 2030, unaolenga kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili, biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu yanayovuka mipaka ya nchi.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni