Breaking


Jumatano, 13 Mei 2026

TASAC NA MSALABA MWEKUNDU WATOA ELIMU YA UOKOAJI NA USALAMA MAJINI KIGOMA


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, limetoa elimu ya uokoaji na usalama majini kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kupunguza ajali zinazotokea katika maeneo ya maji nchini.

Mafunzo hayo yalihusisha elimu ya nadharia pamoja na vitendo kwa wavuvi, waendesha vyombo vya majini, wanafunzi na wananchi wanaotumia usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika. Lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kuhusu hatua za tahadhari na namna ya kujikinga dhidi ya ajali majini.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kigoma, Nahodha Adam Mamilo, amesema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya usalama majini kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa sahihi wa tahadhari zinazotakiwa kuchukuliwa kabla na wakati wa safari za majini.

Ameeleza kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutoa msaada wa haraka pindi ajali zinapotokea, ikiwemo mbinu za uokoaji wa awali, matumizi sahihi ya vifaa vya kujiokoa pamoja na hatua za kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Bw. Exavery Eustarch, amesema mafunzo hayo pia yamejikita katika utoaji wa huduma ya kwanza kwa waathirika wa ajali za majini pamoja na namna ya kushughulikia hali za dharura kabla ya kuwafikisha wahusika katika vituo vya afya.

Wananchi walioshiriki mafunzo hayo wamepongeza juhudi za TASAC na Msalaba Mwekundu kwa kuwapatia elimu muhimu inayosaidia kuokoa maisha na kuongeza usalama katika shughuli zao za kila siku zinazotegemea usafiri wa majini.

Aidha, Nahodha Mamilo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za usalama majini, ikiwemo matumizi ya vifaa vya kuokoa maisha, ili kuhakikisha safari zote za majini zinafanyika kwa usalama wakati wote.


Hakuna maoni: