Breaking


Ijumaa, 22 Mei 2026

TIRDO YAPANUA MAABARA ZA UTAFITI KUKUZA MAENDELEO YA VIWANDA NCHINI


Serikali kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) imeendelea kuimarisha na kuboresha maabara za utafiti kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za kisayansi na kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kapinga amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, maabara ya chakula ya TIRDO iliyopata ithibati mwaka 2025 imeboreshwa zaidi kwa kuongeza wigo wa huduma kutoka huduma tatu hadi sita. Aidha, amesema ongezeko hilo limeenda sambamba na upanuzi wa aina za bidhaa zinazohudumiwa maabarani hapo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika uchunguzi wa bidhaa mbalimbali za viwandani, kuhakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


Mbali na maboresho hayo, Serikali imeeleza kuwa TIRDO inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Maabara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe Region. Mradi huo unatarajiwa kusaidia kusogeza huduma za utafiti karibu na maeneo yenye rasilimali nyingi za madini na shughuli za uzalishaji wa viwandani.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa uwekezaji katika tafiti za kisayansi na teknolojia kama sehemu ya kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

 

Hakuna maoni: