Mganga Mkuu wa Serikali, Grace Magembe, Mei 17, 2026 ameshiriki katika shughuli mbalimbali muhimu zilizotangulia kuanza rasmi kwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHA79) unaotarajiwa kufanyika Mei 18, 2026 mjini Geneva nchini Uswisi.
Katika ushiriki huo, Dkt. Magembe alijumuika na viongozi pamoja na wadau wa afya duniani katika programu ya Walk the Talk, inayolenga kuhamasisha jamii kuzingatia afya bora kupitia mazoezi ya mwili na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na ya mlipuko.Aidha, kwa niaba ya Waziri wa Afya, alihudhuria kikao cha pembeni cha Mawaziri wa Jumuiya ya ECSA-HC kilichofanyika katika Hoteli ya Crowne Plaza Geneva. Kikao hicho kilijadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza ushirikiano wa kikanda pamoja na namna bora ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya katika nchi wanachama.
Katika kikao hicho, Mawaziri wa afya walithibitisha uteuzi wa Ntuli Kapologwe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, hatua inayotarajiwa kuimarisha usimamizi na maendeleo ya sekta ya afya katika ukanda huo.Akizungumza baada ya kushiriki mikutano hiyo, Dkt. Magembe amesema majukwaa ya kimataifa yana nafasi kubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na kujenga mifumo imara ya afya kwa manufaa ya wananchi.
Amesema Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa ya afya ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuimarika sambamba na kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza duniani.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni