Breaking


Jumanne, 12 Mei 2026

UTABIRI WA HALI YA HEWA KWA SAA 24 ZIJAZO

 


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo, Mei 12, 2026, ukionesha kuwepo kwa hali ya mawingu pamoja na mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa utabiri huo, baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani unaojumuisha Visiwa vya Mafia yanatarajiwa kuwa na mawingu pamoja na vipindi vya mvua katika maeneo machache. Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba.


Aidha, mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi sambamba na mvua nyepesi katika baadhi ya maeneo. Katika maeneo ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu pamoja na mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi, hali ya mawingu inatarajiwa kutawala katika vipindi tofauti vya siku.

Kwa upande wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, TMA imesema kutakuwa na hali ya mawingu kiasi huku maeneo machache yakitarajiwa kupata mvua nyepesi. Hali hiyo pia inatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Dodoma na Singida.

Wananchi wametakiwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuchukua tahadhari stahiki, hususan kwa maeneo yanayoweza kupata mvua na radi za hapa na pale.

Hakuna maoni: