Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Afya Duniani wa mwaka 2026 uliofanyika mjini Geneva, Tedros amesema dunia inapaswa kuwa na mshikamano mkubwa katika kukabiliana na changamoto za afya zinazozidi kujitokeza kwa kasi.
Katika hotuba yake, Tedros alizungumzia mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao tayari umetangazwa kuwa dharura ya afya ya kimataifa. Amesema hatua za haraka zinahitajika ili kuzuia maambukizi kusambaa zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Mbali na Ebola, WHO pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu mlipuko wa nadra wa kirusi cha Hanta ulioripotiwa kwenye meli ya kitalii ya MV Hondius. Tukio hilo limeibua mjadala mpya kuhusu usalama wa afya katika safari za kimataifa na umuhimu wa mifumo madhubuti ya tahadhari.
Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ameipongeza nchi yake kwa kuruhusu meli hiyo kutua katika Visiwa vya Canary kwa ajili ya kuwahamisha abiria na wahudumu waliokuwa ndani ya meli hiyo.
Pedro Sánchez amesema hakuna taifa linaloweza kujikinga pekee dhidi ya majanga ya afya duniani, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti milipuko ya magonjwa.
Mkutano wa Afya Duniani wa mwaka 2026 umefanyika katika kipindi ambacho WHO inapitia changamoto kubwa za kifedha baada ya Marekani kutangaza kujiondoa katika baadhi ya michango ya shirika hilo pamoja na kupunguza kiwango cha ufadhili wake.
Wataalamu wa afya duniani wanaamini kuwa ushirikiano wa kimataifa, uwekezaji katika mifumo ya afya, pamoja na utoaji wa taarifa sahihi kwa wananchi ni silaha muhimu katika kukabiliana na magonjwa yanayoendelea kuibuka duniani.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni