Breaking


Jumamosi, 16 Mei 2026

WIZARA YA FEDHA YAKAMILISHA MAFUNZO YA UDHIBITI WA NDANI MOROGORO


Wizara ya Fedha imekamilisha mafunzo ya Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani yaliyolenga kuimarisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi bora wa rasilimali za umma kwa watumishi wa wizara hiyo. Mafunzo hayo yalifanyika katika Hoteli ya Morena mkoani Morogoro yakihusisha Menejimenti ya Wizara pamoja na wataalamu wa ukaguzi wa ndani.

Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Kenneth Nindie, aliwataka washiriki kuhakikisha wanayatekeleza kwa vitendo mafunzo waliyopata katika majukumu yao ya kila siku ili kuongeza ufanisi wa utendaji serikalini.

Alisema kuwa utekelezaji wa mwongozo wa udhibiti wa ndani ni hatua muhimu katika kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za serikali. Aidha, alieleza kuwa mfumo wa udhibiti wa ndani unasaidia kupunguza viatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ndani ya taasisi.

Bw. Nindie alisisitiza kuwa udhibiti wa ndani haupaswi kubaki kuwa nadharia pekee, bali unatakiwa kuzingatiwa na kutekelezwa kwa vitendo katika kila hatua ya kazi ili kuleta matokeo chanya na kuongeza uwazi katika utendaji wa taasisi za umma.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Fedha, Evaristo Mwalongo, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki uelewa mpana kuhusu wajibu wa kila mtumishi kuanzia ngazi za juu hadi za chini katika kusimamia udhibiti wa ndani na kudhibiti viatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yao.

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema itawasaidia kuboresha ufanisi wa kazi na kuongeza uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi. Mafunzo hayo yalijumuisha mada mbalimbali ikiwemo dhana ya udhibiti wa ndani, malengo yake, wajibu wa watumishi na namna ya kusimamia viatarishi katika taasisi za umma.


Hakuna maoni: