Breaking


Ijumaa, 15 Mei 2026

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUTEKELEZA VIPAUMBELE TISA 2026/2027.

Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha sekta ya utalii, uhifadhi wa rasilimali na matumizi ya teknolojia za kisasa katika mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza mapato, ajira na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/2027,Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Ashatu Kijaji,amesema katika mwaka ujao wa fedha serikali itaendelea kuimarisha utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi kwa kutumia mikakati mahsusi ya masoko inayolenga kuvutia watalii kutoka masoko ya kimkakati na mapya, hususan katika nchi za Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati.

Aidha amesema Wizara imepanga kuendeleza na kuboresha mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa meli, mikutano na matukio (MICE), utalii wa fukwe, michezo, anga pamoja na tiba, huku pia ikitambua na kusajili mazao mapya yatakayopanua fursa za uwekezaji, ajira na mapato kwa wananchi.

Serikali pia imeweka mkazo katika kuboresha miundombinu wezeshi katika maeneo ya utalii na hifadhi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano na huduma za kijamii ili kuongeza urahisi wa kufikia vivutio vya utalii na kuboresha huduma kwa watalii.

Dkt.Kijaj amesema katika eneo la uhifadhi, Wizara itaendelea kuimarisha ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale kupitia ushiriki mkubwa wa jamii, kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori, pamoja na kukabiliana na vitendo vya ujangili na uharibifu wa mazingira.

Pia serikali inalenga kuongeza uzalishaji, uongezaji thamani na masoko ya mazao ya misitu na nyuki kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali hizo ili kuongeza mchango wa sekta katika uchumi wa Taifa pamoja na kukuza kipato cha wananchi.

Sambamba na hayo, serikali itafanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta ya maliasili na utalii nchini.

Hakuna maoni: