Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupigia kura vivutio vya utalii vya Tanzania vilivyoingia katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Kimataifa za Utalii Duniani za World Travel Awards 2026, ili viendelee kung’ara kimataifa.
Wito huo umetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, wakati akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini mkoani Njombe kuhusu mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza katika mkutano huo, Msigwa amesema kuwa vivutio mbalimbali vya utalii nchini, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Kitulo na Pori la Akiba la Mpanga-Kipengere, vimefanikiwa kuingia kwenye orodha ya ushindani wa tuzo hizo zinazotambulika duniani.Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayochochea ongezeko la watalii wa ndani na kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Msigwa, ushindi wa vivutio hivyo katika tuzo hizo utasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa, kuongeza idadi ya watalii na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii.“Tunahitaji Watanzania wote kushiriki kupigia kura vivutio vyetu ili viweze kushinda na kuendelea kuitangaza nchi yetu duniani,” amesema Msigwa.
Katika Tuzo za World Travel Awards 2026, Tanzania imefanikiwa kupata zaidi ya uteuzi 85 katika vipengele 41 tofauti, jambo linaloonesha namna sekta ya utalii nchini inavyoendelea kukua na kupata kutambuliwa kimataifa.Aidha, katika kipengele cha Africa’s Leading Tourist Attraction 2026, Tanzania imeweka rekodi kwa kuingiza vivutio saba kati ya vivutio 14 vilivyoteuliwa barani Afrika, hatua inayodhihirisha ubora wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Sekta ya utalii inaendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania kupitia mapato ya fedha za kigeni, ajira na maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi na vivutio vya asili.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni