Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mheshimiwa Balozi Saidi Othman Yakubu, amekutana na Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi wa Dunia cha UNESCO, Bw. Lazare Eloundou Assomo, katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris kwa mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya urithi wa dunia.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNESCO katika uhifadhi, ulinzi na usimamizi endelevu wa maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyopo nchini Tanzania pamoja na fursa za kuongeza ushirikiano wa kiufundi na kujengeana uwezo katika sekta hiyo muhimu.
Balozi Yakubu alisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuhifadhi na kuendeleza urithi wake wa kipekee wa asili na utamaduni, ukiwemo urithi uliotambuliwa na UNESCO, huku akieleza umuhimu wa urithi huo katika kukuza utalii, maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Bw. Assomo alieleza utayari wa UNESCO kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika kuhakikisha maeneo ya urithi wa dunia yanaendelea kulindwa na kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Mazungumzo hayo pia yaligusia maandalizi ya mikutano ya Kamati ya Urithi wa Dunia, ushiriki wa nchi za Afrika katika agenda za urithi wa dunia, pamoja na umuhimu wa kuimarisha uwakilishi wa bara la Afrika katika mifumo ya kimataifa ya uhifadhi wa urithi wa dunia.
Mwisho wa mazungumzo hayo, pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na UNESCO kwa manufaa ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa urithi wa dunia.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni