Breaking


Jumamosi, 13 Juni 2026

NGOMA ZA ASILI ZANG’ARA UMITASHUMTA 2026, ZAENDELEA KUENZI UTAMADUNI WA TANZANIA


Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) 2026 yameendelea kung’ara mkoani Iringa, huku vikundi vya ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali vikionesha vipaji, ubunifu na urithi wa tamaduni za Tanzania kupitia maonesho ya sanaa za jadi.

Maonesho hayo yalifanyika Juni 12, 2026, katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Klerruu, Manispaa ya Iringa, ambapo wanafunzi walipata fursa ya kuwasilisha ngoma mbalimbali za asili zinazowakilisha mila, desturi na historia za jamii tofauti nchini. Ushiriki huo umeendelea kuwa sehemu muhimu ya kukuza na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Mratibu wa Sanaa za Maonesho wa UMITASHUMTA 2026, Bi. Leah Kihimbi, alisema kuwa kuwashirikisha watoto katika sanaa za maonesho ni njia bora ya kuwajengea uelewa wa utamaduni wao tangu wakiwa wadogo.

Alieleza kuwa wanafunzi wanaposhiriki katika ngoma za asili na shughuli nyingine za kitamaduni, hupata fursa ya kujifunza historia, mila na desturi za jamii zao, jambo linalochangia kujenga kizazi kinachojivunia na kuthamini urithi wa Taifa.

Bi. Kihimbi pia alibainisha kuwa ushindani wa mwaka huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, hali inayoonesha jitihada zinazofanywa na mikoa mbalimbali katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya sanaa kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Mbali na kuwa jukwaa la ushindani, maonesho ya ngoma za asili yameendelea kuwa fursa ya wanafunzi kujifunza na kubadilishana uzoefu wa tamaduni mbalimbali zinazopatikana nchini. Watazamaji na washiriki wameendelea kuvutiwa na ubora wa maonesho hayo, ambayo yameonyesha utajiri mkubwa wa utamaduni wa Tanzania.

UMITASHUMTA 2026 inaendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji vya watoto katika michezo na taaluma, huku ikichangia pia kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni wa Taifa kwa vizazi vijavyo.


Hakuna maoni: