Akizungumza akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 11 ya wahitimu wa Kidato cha Nne (Year 11–IGCSE) wa mwaka wa masomo 2025/2026 wa Shule ya Kimataifa ya Feza yaliyofanyika Salasala, Dar es Salaam, Juni 12, 2026, Dkt. Mwigulu alisema Serikali inatambua nafasi muhimu ya sekta binafsi katika kuendeleza elimu nchini.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu hayawezi kutenganishwa na mchango wa shule binafsi, hususan Taasisi ya Feza ambayo imekuwa miongoni mwa taasisi zilizoweka viwango vya juu vya ubora wa elimu vinavyotambulika ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, shule za Feza zimechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya elimu nchini na kuwa mfano wa utoaji wa elimu bora inayokidhi viwango vya kimataifa. Alibainisha kuwa taasisi hiyo imeendelea kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali duniani, jambo linalodhihirisha ubora wa huduma za elimu zinazotolewa.
Dkt. Mwigulu pia alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali katika sekta ya elimu kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo inalenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora na kuifanya elimu ya lazima kuwa ya miaka 10. Alisema hatua hiyo inalenga kuwaandaa vijana wa Kitanzania kukabiliana na mabadiliko ya dunia ya sasa pamoja na mahitaji ya sayansi na teknolojia.Aidha, ameipongeza Taasisi ya Feza kwa mchango wake katika shughuli za uwajibikaji kwa jamii ikiwemo kusaidia wanafunzi wenye uhitaji, kuboresha miundombinu ya shule za umma na kuchangia upatikanaji wa huduma za maji kupitia uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Akizungumzia umuhimu wa elimu katika maendeleo ya Taifa, Waziri Mkuu alisema uwekezaji katika rasilimali watu ndiyo nguzo kuu ya maendeleo endelevu. Alisisitiza kuwa nchi yenye watu wenye maarifa, ujuzi na maadili inaweza kufikia maendeleo makubwa hata kama haina rasilimali nyingi za asili.
Kwa upande wake, aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kwa manufaa ya jamii na Taifa, kudumisha nidhamu, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kwa njia yenye tija. Alisema mafanikio ya kweli hayatapimwa kwa matokeo ya mitihani pekee bali kwa mchango wao katika kuijenga jamii na Taifa kwa ujumla.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni