Timu ya mpira wa miguu ya Albinism SC inatarajiwa kushuka dimbani tarehe 6 Juni 2026 jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri kucheza dhidi ya Bunge SC katika mchezo maalum unaolenga kuongeza uelewa kuhusu ualbino na kuhamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ualbino katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Mchezo huo pia ni sehemu ya hamasa kuelekea Mbio za Kimataifa za Ualbino zinazotarajiwa kufanyika mkoani Mara baadaye mwaka huu.
Akizungumza katika ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wakati wa kukamilisha uratibu wa safari kuelekea Dodoma, Katibu wa Klabu ya Albinism SC, Bw. Joseph Sinda amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa katika kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki, uwezo na mchango wa watu wenye ualbino katika maendeleo ya taifa.
Bw. Sinda amelishukuru Baraza la Michezo la Taifa kwa kuwezesha safari ya timu hiyo, hatua ambayo imechangia maandalizi mazuri ya ushiriki wao katika mchezo huo muhimu.
Mchezo huo unatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa michezo na jamii kwa ujumla katika kuendeleza ujumbe wa usawa, ujumuishi na fursa sawa kwa wote.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni