Breaking


Alhamisi, 11 Juni 2026

DKT. MAULID ASISITIZA UONGOZI WA KIMKAKATI KATIKA USIMAMIZI WA SEKTA YA ELIMU


Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid Maulid, amesisitiza umuhimu wa uongozi wa kimkakati katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya elimu nchini, akieleza kuwa viongozi wenye maono na uwezo wa kupanga mikakati bora ni msingi wa kuboresha utendaji wa shule na matokeo ya wanafunzi.


Dkt. Maulid ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya uongozi wa kimkakati kwa viongozi wa shule za sekondari wa Manispaa ya Shinyanga. Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki 44, wakiwemo Wakuu wa Shule za Sekondari 22 na Makamu Wakuu wa Shule 22.



Mafunzo hayo yanatekelezwa na ADEM kwa kushirikiana na African Centre for School Leadership (ACSL) kupitia VVOB, kwa ufadhili wa Mastercard Foundation, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa viongozi wa elimu katika kusimamia taasisi zao kwa ufanisi zaidi.


Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Maulid amesema kuwa uongozi wa kimkakati una mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta ya elimu na kuongeza uwajibikaji katika taasisi za umma.


Aidha, ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatumia mbinu za kisasa za ufundishaji zinazowapa washiriki fursa ya kujifunza kwa vitendo, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa yatakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuongozi katika maeneo yao ya kazi.


Katika hatua nyingine, Dkt. Maulid amesisitiza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa maarifa na ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo hayo. Amesema mafanikio ya programu hiyo yatapimwa kwa kuangalia mabadiliko chanya yatakayojitokeza katika usimamizi, uendeshaji na utendaji wa shule zinazoshiriki.


Wadau wa elimu wanaamini kuwa mafunzo ya aina hii yanaweza kuchangia kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha uwezo wa viongozi wa shule katika kufanya maamuzi sahihi, kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kuendeleza mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Hakuna maoni: