Breaking


Jumanne, 9 Juni 2026

FIFA YAMWONDOA MWAMUZI WA SOMALIA OMAN ABDULKADIR ARTAN KWENYE KOMBE LA DUNIA 2026


Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limethibitisha kuwa mwamuzi kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan, hatahusika katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya FIFA, Artan alizuiwa kuingia Marekani mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami. Baada ya mawasiliano na mamlaka za uhamiaji za Marekani, FIFA ilithibitisha kuwa mwamuzi huyo hataruhusiwa kushiriki mafunzo wala kuchezesha mechi zozote za mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

“FIFA inaweza kuthibitisha kuwa mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hataweza kushiriki mafunzo wala kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

FIFA imefafanua kuwa haihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji wa mashindano, ikiwemo masuala ya utoaji wa viza na vibali vya kuingia nchini. Aidha, mamlaka husika zimeeleza kuwa hali ya mwamuzi huyo haitabadilika kwa sasa.

Hadi sasa, mamlaka za Marekani hazijatoa sababu rasmi ya hatua hiyo. Hata hivyo, Somalia ni miongoni mwa nchi zilizowahi kuwekwa kwenye orodha ya vizuizi vya usafiri iliyoanzishwa wakati wa utawala wa Donald Trump.

Hatua hiyo imezua mjadala miongoni mwa wadau wa soka kuhusu athari za sera za uhamiaji kwa ushiriki wa waamuzi, wachezaji na maafisa wa michezo katika matukio makubwa ya kimataifa kama Kombe la Dunia 2026.


Hakuna maoni: