Breaking


Alhamisi, 25 Juni 2026

HOSPITALI KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOANI MARA KUKAMILIKA FEBRUARI 2027



Serikali imesema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2027, hatua itakayoongeza uwezo wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Musoma Mjini na maeneo jirani.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma leo Juni 25, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Musoma Mjini, Mhe Mgore Miraji Kigera, aliyetaka kujua lini Serikali itakamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.

Dkt. Samizi amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa Wing A, B na C na unatekelezwa kwa awamu tano, ambapo awamu ya kwanza hadi ya nne zimekamilika na kufanya Wing B na C kuanza kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Amesema Serikali imeingia mkataba wa shilingi bilioni 20.2 kwa ajili ya kukamilisha Wing A, inayojumuisha Idara ya Wagonjwa wa Nje, Famasi, Idara ya Dharura, Maabara, Wodi za Wanaume na Watoto, Idara ya Kinywa na Meno, ofisi za utawala pamoja na kazi za uunganishaji wa umeme mkubwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Samizi, mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 5.5 kama malipo ya awali na utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 58.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi.

Hakuna maoni: