Breaking


Jumatano, 3 Juni 2026

MRADI WA FOLUR KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA VIWANGO VYA KIMATAIFA ZANZIBAR

Mradi wa Mifumo ya Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho wa Mandhari ya Misitu nchini Tanzania (FOLUR) unatarajia kutoa mafunzo maalum kwa viongozi wa serikali za vijiji, shehia na maafisa ugani wa kilimo na misitu Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kuzingatia viwango na miongozo ya kimataifa.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa ngazi za jamii ili waweze kutambua, kuzuia na kupunguza athari za kimazingira na kijamii zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli za mradi.

Akifungua mafunzo kwa maafisa ugani wa kilimo na misitu Zanzibar, Mratibu wa Mradi wa FOLUR, Bi. Miza Suleiman Khamis, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha shughuli zote za mradi zinatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitengo cha Jinsia, Usalama wa Mazingira na Jamii wa mradi huo, Bw. Revocatus Kadoshi, alisema washiriki watapatiwa elimu kuhusu miongozo minne muhimu inayosimamia utekelezaji wa miradi ya mazingira na maendeleo.

Alitaja mojawapo ya miongozo hiyo kuwa ni Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na Jamii (ESMP), unaolenga kudhibiti matumizi ya rasilimali kwa ufanisi, kupunguza athari za mazingira na kuzuia uhamishaji wa watu usio wa hiari wakati wa utekelezaji wa miradi.

Kwa mujibu wa Bw. Kadoshi, mwongozo huo unaendana na sera na taratibu za kimataifa za ulinzi wa kijamii zinazotumiwa na mashirika mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira duniani, ikiwemo WWF.

Aidha, washiriki watafundishwa kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Visumbufu, mfumo unaolenga kulinda afya na usalama wa jamii kwa kudhibiti athari zinazoweza kusababishwa na matumizi ya viuatilifu na mbolea katika shughuli za kilimo.

Mafunzo hayo pia yatahusisha mbinu bora za usimamizi wa mazingira, usalama mahali pa kazi, pamoja na kudumisha usafi wa mazingira katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.

Sambamba na hilo, mradi wa FOLUR umeweka utaratibu maalum wa kupokea na kushughulikia malalamiko kutoka kwa wananchi na makundi mbalimbali ya kijamii kuhusu shughuli zinazotekelezwa na mradi. Mfumo huo unalenga kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi na kupata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo au malalamiko wakati wowote inapohitajika.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya mradi wa FOLUR katika kuhakikisha maendeleo ya kilimo, matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa mazingira yanaenda sambamba na maslahi ya wananchi pamoja na viwango vya kimataifa vya uendelevu.


Hakuna maoni: