Mkoa wa Mwanza umetajwa kuwa Kinara kwa kuratibu na kusimamia ipasavyo shughuli za kukabiliana na maafa, majanga na mawasiliano ya dharura kutokana na hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura.
Sifa hizo zimetolewa Juni 4, 2026 na wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mafunzo ya Kamati za Usimamizi wa Maafa yanayofanyika mkoani Mwanza kwa siku mbili yakilenga kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amesema maafa yameendelea kuwa tishio kubwa duniani kutokana na athari zake kwa maisha ya watu, uchumi na maendeleo ya jamii na kuzitaka Wilaya zote Mkoani humo kuwa na mipango kazi na mifumo imara ya usimamizi wa maafa ili kuhakikisha maandalizi, mwitikio wa haraka na urejeshaji wa hali unafanyika kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha usimamizi wa maafa kwa kutumia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2024 pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa eneo la utafiti kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Vanvaco Luvanda amesema mafunzo hayo ya siku mbili yanaendelea kutolewa nchini kote kwa lengo la kuongeza utayari na uwezo wa kitaalamu wa kukabiliana na maafa yanapotokea.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni