NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema Serikali itaendelea kukitambua na kushirikiana na Chama cha Wapagazi (Tanzania Association of Porters – TAP) kama mdau muhimu wa kuongoza watalii kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini
Mhe. Chande amesema hayo leo Juni 8, 2026, katika Bunge la 13, Mkutano wa tatu, Kikao cha 45, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Mhe. Ibrahim Mohamed Shayo (CCM), aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kukitambua chama hicho na kukishirikisha kama mdau muhimu wa utalii nchini
“Wizara inakitambua chama hiki na imekuwa ikishirikiana nacho katika matukio mbalimbali yanayohusu Wapagazi ikiwemo ushiriki wa vikao vya wadau vilivyofanyika jijini Dodoma na mafunzo kwa wapagazi yaliyoandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TATO) yaliyofanyika Mei 11, mwaka huu, jijini Arusha na Mei 13, mwaka huu katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro,” amesisitiza Mhe. Chande.
Katika hatua nyingine Mhe. Chande amempongeza Mbunge huyo kwa kukubali kuwa mlezi wa chama hicho cha Wapagazi Tanzania na kumhakikishia kuwa Wizara itaendelea kumpatia ushirikiano katika kutimiza jukumu hilo la kuendeleza Sekta ya Utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa fursa za ajira kwa vijana, Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni