Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema hatua hiyo inatekelezwa kupitia Sheria ya Uvuvi, Sura ya 279 pamoja na Sheria ya Usimamizi na Uendelezaji wa Uvuvi katika Bahari Kuu, Sura ya 388, ambazo zimeweka mfumo wa kulinda ushiriki wa wazawa katika shughuli mbalimbali za uvuvi.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Regina Christopher Malima, bungeni jijini Dodoma Juni 10, 2026, Waziri Bashiru alisema sheria hizo zimezuia wageni kushiriki baadhi ya shughuli za uvuvi katika maji ya ndani na biashara ya baadhi ya mazao ya uvuvi, ili kutoa nafasi zaidi kwa Watanzania kunufaika na sekta hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa unafuu wa gharama za leseni na tozo mbalimbali kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi pamoja na ufugaji samaki kwa vizimba. Hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wazawa na kuwawezesha kushindana katika mazingira ya haki na usawa.Kwa mujibu wa Waziri huyo, sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kupitia ajira, usalama wa chakula na uzalishaji wa bidhaa za uvuvi, hivyo Serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayochochea ukuaji wa sekta hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, Serikali imeahidi kuendelea kufanya maboresho ya sheria na kanuni pale inapobidi, ili kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa na fursa za uwekezaji katika sekta ya uvuvi zinawanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa zaidi.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni