Breaking


Ijumaa, 12 Juni 2026

SERIKALI YASISITIZA UMUHIMU WA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA.


SERIKALI imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya uadilifu katika utumishi wa umma ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu na mipango ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ameeleza hayo Juni 12,2026,Jijini Arusha wakati akifungua Mafunzo ya Kamati ya Uadilifu yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati Maalum ya Menejimenti katika kusimamia masuala ya uadilifu katika ofisi hiyo.

Dkt. Yonazi amesema uadilifu ni nguzo muhimu katika ufanikishaji wa majukumu hivyo ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuhakikisha anazingatia maadili ya kazi na kulinda misingi ya uadilifu ili kuimarisha utendaji na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.

Dkt. Yonazi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wajumbe kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Uadilifu kwa kuhakikisha unaingizwa katika mipango kazi na bajeti za mwaka za taasisi.

Akiwasilisha mada ya masuala ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP IV) 2023-2030 Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Ikulu Andrew Massawe amesema, ni wajibu wa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kupinga vitendo vyote vinavyoashiria mazingira ya rushwa ili kuendelea kuhudumia wananchi, na Taifa kwa ujumla katika misingi sahihi ya utumishi wa umma.

Hakuna maoni: