Takwimu hizo zimetolewa Juni 12, 2026 na Mtakwimu Mwandamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mdoka Omary, wakati wa kikao kazi cha uratibu wa shughuli za watu wenye ulemavu kilichowakutanisha waratibu wa madawati ya watu wenye ulemavu kutoka wizara mbalimbali jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mdoka amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa Tanzania ina watu wenye ulemavu 5,347,397, ikilinganishwa na milioni 3.2 zilizorekodiwa mwaka 2012. Amesema ongezeko hilo limetokana na maboresho ya mbinu za ukusanyaji wa takwimu pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi wakati wa sensa na tafiti mbalimbali.Aidha, Serikali imeboresha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za watu wenye ulemavu kwa kujumuisha aina mbalimbali za ulemavu, taarifa za chanzo chake pamoja na matumizi ya vifaa saidizi. Mfumo wa takwimu za kiutawala pia umeanza kutumika katika mikoa 16 ya Tanzania Bara kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa wakati kwa watunga sera na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Vedastina Justiniani, amesema Serikali imepiga hatua kubwa kupitia madawati ya watu wenye ulemavu yaliyopo katika wizara mbalimbali. Amesema madawati hayo yameongeza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika programu za maendeleo na huduma za Serikali.Vedastina ameongeza kuwa Serikali inaendelea kusimamia utoaji wa mikopo kwa makundi maalum kupitia halmashauri mbalimbali nchini pamoja na kuendeleza zoezi la usajili wa watu wenye ulemavu kwa lengo la kujenga kanzidata sahihi itakayosaidia katika upangaji na utoaji bora wa huduma.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Jerode Komba, amesema Serikali itaendelea kujenga uwezo wa watumishi wanaohudumia watu wenye ulemavu na kupanua madawati hayo katika taasisi nyingine za umma ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha ustawi wa watu wenye ulemavu kwa kuimarisha mifumo ya takwimu, upatikanaji wa huduma na fursa za kiuchumi, sambamba na kuongeza ushirikishwaji wao katika shughuli za maendeleo ya taifa.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni