Singapore imeipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi Barani Afrika, ikiwa na idadi kubwa ya vijana, rasilimali asilia, na nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi.
Mbali na hilo, Singapore imesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inaonesha dhamira ya Tanzania kuingia katika hatua mpya ya ukuaji.
Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, ametoa pongezi hizo Ikulu jijini Dar es salaam, wakati wa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Rais wa Singapore, ameupongeza uongozi wa Rais Dokta Samia katika kufungua maeneo mapya ya ushirikiano na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kati ya Afrika Mashariki na Asia.
Biashara kati ya nchi hizo imefikia dola za Marekani Milioni-299, huku Singapore ikiwa na miradi 36 ya uwekezaji nchini Tanzania.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Singapore, Tharman, ameelekea
Visiwani Zanzibar, ambapo atafanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi.
Baada ya hapo atakutana na Waandishi wa Habari wa Singapore.
Aidha, atarejea jijini Dar es salaam Saa 12 jioni na ataondoka nchini Saa 4 usiku katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akielekea Uholanzi.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni