Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema takwimu rasmi zitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Daniel Masolwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo NBS inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika maonesho hayo, Masolwa amesema takwimu rasmi ni msingi wa upangaji wa maendeleo na husaidia serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau mbalimbali kufanya maamuzi sahihi yanayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.
Ameeleza kuwa NBS huzalisha takwimu mbalimbali zinazotumika katika sekta tofauti za uchumi na maendeleo. Takwimu hizo ni pamoja na za mfumuko wa bei zinazotolewa kila mwezi, takwimu za Pato la Taifa (GDP) zinazotolewa kwa vipindi vya robo mwaka, pamoja na takwimu za ajira zinazoonesha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wa ajira na nguvu kazi iliyopo nchini.
Aidha, amesema taasisi hiyo huzalisha takwimu za kilimo, uzalishaji viwandani, biashara ya nje, pamoja na takwimu za kijamii zinazopatikana kupitia Sensa ya Watu na Makazi, ambazo husaidia kutathmini maendeleo ya wananchi na kupanga mikakati ya baadaye.
Masolwa amesisitiza kuwa NBS itaendelea kuhakikisha takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa na kwa uwazi unaohitajika ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika utaendelea kuwa chachu ya maendeleo, uwekezaji na uboreshaji wa huduma za kijamii, huku ukiiwezesha Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi mkubwa, shindani na unaowanufaisha wananchi wote.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni