Breaking


Alhamisi, 18 Juni 2026

TASAF YATAJWA KUBADILI MAISHA YA WANUFAIKA, AWAMU YA TATU KULETA MABORESHO ZAIDI


Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wamesema kuwa mpango huo umekuwa msaada mkubwa katika kuboresha maisha yao na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Wanufaika hao walitoa kauli hiyo walipotembelea banda la TASAF katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akizungumza katika maonesho hayo, Fatma Ally Mohamed kutoka Unguja, Zanzibar, alisema TASAF imemsaidia kuboresha hali ya maisha ya familia yake baada ya kupitia changamoto mbalimbali za kiuchumi. Kauli kama hiyo ilitolewa na Zuwena Hamis kutoka Temeke, Dar es Salaam, ambaye alisema mpango huo umekuwa chachu ya maendeleo kwa kaya yake.

Wanufaika hao walieleza kuwa kabla ya kujiunga na mpango huo walikabiliwa na hali ngumu za maisha, lakini kwa sasa wamepata fursa ya kuboresha ustawi wa familia zao kupitia msaada na uwezeshaji unaotolewa na TASAF.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF, Godwin Mkisi, amesema awamu ya tatu ya mpango huo inalenga kuleta maboresho zaidi katika utekelezaji wake ili kuongeza manufaa kwa wananchi.

Aidha, Mkisi alibainisha kuwa pamoja na juhudi za kupunguza umasikini, TASAF itaendelea kushiriki katika mikakati ya kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoathiri jamii, hatua ambayo inalenga kuimarisha ustahimilivu wa kaya na kuchangia maendeleo endelevu ya wananchi.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameendelea kutoa fursa kwa taasisi mbalimbali za umma kuwasilisha huduma, mafanikio na mipango yao kwa wananchi, huku TASAF ikitumia jukwaa hilo kueleza mchango wake katika kuboresha maisha ya Watanzania.


Hakuna maoni: