Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Kakurwa, amekutana na kufanya mazungumzo na Chama cha Umoja wa Wafugaji Samaki Tanzania kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati bora ya ushirikiano kati ya chama hicho na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuendeleza sekta ya ufugaji samaki nchini.
Mazungumzo hayo yamefanyika Juni 23, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi Kambarage jijini Dodoma, ambapo pande zote mbili zimejadili fursa, changamoto na mikakati ya kuimarisha uzalishaji wa samaki pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Kakurwa amekipongeza chama hicho kwa juhudi zake za kuwaunganisha wafugaji samaki nchini na kuwataka wanachama wake kuendeleza umoja, nidhamu, hekima na ushirikiano ili kuhakikisha chama kinaendeshwa kwa weledi na kuleta matokeo chanya kwa wanachama na sekta kwa ujumla.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi na ufugaji samaki katika kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji, kuongeza uzalishaji na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kufikia malengo ya maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, Mhe. Waziri amesisitiza umuhimu wa chama hicho kushiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni na ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala yanayohusu ufugaji samaki vilevile amebainisha kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau ni msingi muhimu wa kukuza sekta na kuongeza ajira pamoja na kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Wafugaji Samaki Tanzania, Bw.Baraka Kalangahe, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kutoa ushirikiano na nafasi ya kusikiliza maoni ya wafugaji samaki, amesema chama hicho kiko tayari kushirikiana na wizara katika kutekeleza mikakati mbalimbali itakayosaidia kuimarisha ufugaji samaki na kuongeza uzalishaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni