Wakala wa Vipimo (WMA) umeendelea kuvutia wadau na wananchi mbalimbali wanaotembelea banda lake katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Uwanja wa Chinangali jijini Dodoma. Wageni wengi wametaja elimu inayotolewa kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kuwa muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi na kulinda haki za watumiaji wa bidhaa na huduma.
Katika siku ya kwanza ya maadhimisho hayo yaliyianza Juni 16, 2026, baadhi ya wageni waliotembelea banda la WMA walieleza kuridhishwa na maelezo wanayopata kutoka kwa wataalamu wa taasisi hiyo. Walisema elimu hiyo imewasaidia kufahamu umuhimu wa vipimo sahihi katika shughuli za biashara, huduma na maisha ya kila siku.Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni Nadhifa Nyoni kutoka TANGA UWASA, Rose Mmary kutoka JWTZ pamoja na Janeth Matara, mkazi wa Dodoma. Wote walipongeza juhudi za WMA katika kusimamia usahihi wa vipimo na kutoa elimu kwa umma, wakisema hatua hiyo inachangia kujenga uaminifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Naye mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Abbas Kayanda, aliipongeza WMA kwa kazi inayofanya huku akishauri kuongezwa kwa kampeni za elimu kwa wananchi wengi zaidi, hasa katika maeneo ya vijijini. Alisema upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu vipimo utasaidia wananchi kuelewa haki zao na kufanya maamuzi bora wanaponunua bidhaa au kupata huduma mbalimbali.Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yataendelea hadi Juni 23, 2026, yakiwakutanisha taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kuonesha huduma wanazotoa na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na wananchi. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “KUCHOCHEA UWAJIBIKAJI JUMUISHI KWA MAENDELEO ENDELEVU,” ikilenga kuhimiza uwazi, ushirikishwaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni