Breaking


Jumamosi, 11 Julai 2026

JKCI NA BMH WAIMARISHA UTALII TIBA

Watoto kutoka nchini Burundi waliokuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na watalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete -JKCI  kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) hatua inayoendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba Barani Afrika.

Upasuaji huo umefanyika katika kambi maalumu yenye malengo ya kuweka ushirikiano baina ya wataalamu hao, kubadilishana ujuzi pamoja na kuonesha umahiri wa wataalamu wa Tanzania katika kutoa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo kwa watoto.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Profesa Abel Makubi alisema mafanikio ya kambi hiyo yameonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kutoa huduma za kibingwa kwa kushirikiana huku ikidhihirisha matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya.

Profesa Makubi alisema kambi hiyo ni mwanzo wa ushirikiano kati ya BMH na JKCI ukiwa na dhumuni la kuongeza upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo kwa watanzania na watu kutoka katika mataifa mengine.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema ushirikiano huo umeiwezesha timu za wataalamu wa upasuaji wa moyo kubadilishana uzoefu na kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kibingwa.

Naye Mratibu wa Utalii Tiba kutoka Wizara ya Afya Dokta Asha Mahita alisema mafanikio ya kambi hiyo yanaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyolenga kuifanya Tanzania  kuwa kitovu cha tiba utalii Barani Afrika.

Hakuna maoni: