Breaking


Alhamisi, 16 Julai 2026

KAMATI YA KITAIFA YA UFUNGAJI MIGODI YAPITIA MPANGO WA UFUNGAJI WA MGODI WA BULYANHULU

Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imeendelea na vikao vyake kwa kupitia Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

Lengo la kikao hicho lilikuwa kupitia, kujadili na kutathmini iwapo mpango huo unakidhi matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, Kanuni za Uchimbaji Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za Mwaka 2010, pamoja na Mwongozo wa Ufungaji Migodi wa Mwaka 2019.

Akiongoza kikao hicho kilichowakutanisha wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Madini, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini, pamoja na viongozi wa Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema migodi ya kati na mikubwa inalazimika kisheria kuandaa na kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio na uidhinishaji.

Mhandisi Kamando amesema jukumu la Kamati hiyo ni kupitia na kuidhinisha mipango ya ufungaji migodi ili kuhakikisha kuwa, shughuli za uchimbaji zinapofikia mwisho, utekelezaji wa mpango huo unaacha mazingira salama, yanayorejeshwa katika hali inayokubalika, pamoja na kulinda ustawi wa jamii zinazozunguka migodi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, Agapith Paul, ameishukuru Kamati kwa maoni na ushauri uliotolewa, akisema utasaidia kuboresha Mpango wa Ufungaji wa Mgodi huo. 

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni, amesema uwepo wa migodi mkoani humo umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa ajira kwa vijana, kuongeza fursa kwa wazabuni na wakandarasi wazawa, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Shinyanga.

Hakuna maoni: