Tanzania imeendelea kuimarisha hatua za kukabiliana na changamoto ya utapiamlo huku ikidhibiti ongezeko la unene uliopitiliza, kiribatumbo na magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na lishe duni ili kupunguza athari za kiafya na kiuchumi zitokanazo na magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wakati akiwasilisha mafanikio na changamoto, na mikakati ya Tanzania katika mjadala wa viongozi wa serikali uliofanyika kwenye Kongamano la Kimataifa kuhusu Unene uliopitiliza (International Congress on Obesity – ICO) nchini Mexico.
Dkt. Magembe amesema moja ya hatua muhimu zinazotekelezwa na Serikali ni kuhamasisha wananchi kubadili mtindo wa maisha kupitia kampeni ya "Zijue Namba Zako" iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa ikilenga kuwahamasisha wananchi kupima mara kwa mara shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uzito, urefu na mzunguko wa kiuno ili kubaini mapema viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza na kuchukua hatua za kinga na matibabu.
Amesema pamoja na hatua hizo, Serikali imewekeza katika kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaowezesha kufanya maamuzi sahihi ya kisera, ikiwemo kuandaa Tathmini ya Kitaifa ya Uwekezaji katika Kuzuia Uzito Uliozidi na Unene, kufanya tathmini ya ubora wa lishe wa vyakula vilivyofungashwa vinavyopatikana sokoni pamoja na tafiti za uelewa wa watumiaji kuhusu taarifa za lishe zinazowekwa kwenye vifungashio vya bidhaa.
Aidha, amesema Tanzania imeandaa Mfumo wa Kitaifa wa Kutathmini Ubora wa Virutubisho kwenye Vyakula na kushiriki katika kuandaa Mfumo wa Pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kutathmini Ubora wa Virutubisho kwenye Vyakula, ambao utakuwa msingi wa kuandaa sera za kuweka alama za tahadhari kwenye vifungashio vya vyakula, kudhibiti matangazo ya vyakula vyenye madhara kiafya hasa kwa watoto na kuboresha mazingira ya lishe shuleni.
Dkt. Magembe amesema mafanikio hayo yamewezekana kutokana na ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti, vyuo vya elimu ya juu, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, ambapo maamuzi yote yamejengwa juu ya ushahidi wa kisayansi na ushirikiano wa kisekta.
Kongamano hilo linatarajiwa kuendelea hadi Julai 17, 2026, likitoa fursa kwa nchi zinazoshiriki kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za kuzuia unene uliopitiliza na kiribatumbo pamoja na kutambua fursa za kupata rasilimali fedha za kutekeleza afua za kuzuia unene uliopitiliza, viriba tumbo na magonjwa yasiyoambukiza.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni