Breaking


Alhamisi, 16 Julai 2026

TAFITI ZA MALIKALE KUCHOCHEA UTALII NA DIPLOMASIA YA UCHUMI



NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ameisihi jamii kujikita katika shughuli mbalimbali za uhifadhi na  utafiti wa mabaki ya kihistoria na urithi wa Malikale ili kusaida katika kukuza diplomasia ya uchumi na pato la taifa kupitia utalii wa maeneo ya Malikale yaliyopo hapa nchini.

Mhe. Chande amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara maalum katika Makumbusho ya Taifa la Tanzania ili kufanikisha lengo la uhifadhi wa kihistoria na urithi wa Malikale na kupata fursa ya kuzungumza na watafiti  wa mabaki ya kihistoria kwa lengo la kusaidia kuongeza ufanisi wa Makumbusho hayo.

“Utafiti ndiyo ukombozi wa kila kitu, unapofanya shughuli yoyote kupitia utafiti, mafanikio yake ndio yanaweza kuonekana, kwa hiyo nitoe wito kwa wananchi wote wasomi na wasio wasomi kutembelea maeneo yetu ya Makumbusho kujifunza historia yetu na wale waliopo vyuoni waje kufanya tafiti,” alisema Mhe. Chande.

Amesema nia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuboresha miundombinu katika taasisi hiyo ya Makumbusho ya Taifa ili kuchochea tafiti na ongezeko la utalii wa kihistoria kwa kuwavutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kufikia idadi ya wataliii milioni 8 ifikapo 2030.

Mhe. Chande, ameelekeza Menejimenti ya taasisi hiyo kutumia mifumo ya kisasa kulingana na teknolojia iliyopo katika kuhifadhi taarifa za kihistoria ili kuwawezesha wageni kupata taarifa muhimu kwa ufasaha bila kupoteza muda. 

Aidha, ameelekeza taasisi hiyo ikamilishe mfumo utakaotumiwa na watalii kupanga safari na kulipia kabla hajafika ukamilike na uanze kutumika mapema iwezekanavyo huku akisisitiza Watanzania kila mmoja kutumia vyema mashindano yajayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) katika kutangaza utalii wa Malikale ndani na nje ya nchi.

Mhe. Chande ameongeza kuwa Serikali ipo tayari kufanya marekebisho ya kanuni za Malikale ili kuwavutia wawekezaji kwenye maeneo hayo  ili kuifanya Makumbusho kuwa sehemu muhimu ya uchumi kwa maslahi mapana na maendeleo ya taifa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania Dkt. Noel Biseko Lwoga amesema taasisi hiyo inakwenda kufanyia kazi maelekezo ya Wizara kwa kupitia miradi miwili ya kimkakati ikiwemo kujisajili kwa watalii kupitia fomu ya malipo mtandaoni na kujisajili kidigital (Self Service Portal) itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa haraka kwa watalii na ongezeko la mapato kwenye taasisi hiyo.

“Maonesho yetu bado yana mfumo wa zamani, lakini sasa tumeweka baadhi ya screen kwa ajili ya kumfanya mgeni kuelewa historia ya nchi yetu na maswala mbalimbali kupitia teknolojia ya kisasa badala ya kuweka taarifa hizo kwenye makaratasi,” amesema Dkt. Lwoga.


Pamoja na mambo mengine Mhe. Chande amepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chimbuko na asili ya binadamu, ndege ya kwanza kutumika na Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na namna ilivyotumika kusaida ukombozi wa baadhi ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika, na alitembelea Kijiji cha Makumbusho kujionea shughuli za jadi na utamaduni wa Mtanzania. 

Hakuna maoni: