Breaking


Alhamisi, 9 Julai 2026

SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA MIRADI KWA NJIA YA UBIA



Serikali imesema itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ikiwemo miundombinu ya usafiri ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali na kwa wakati.

Hayo yalielezwa na Kaimu Kamishna, Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPU), Wizara ya Fedha, Bw. Bashiru Taratibu, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Alisema Serikali imefanya maboresho ya Sera, Sheria na Kanuni za PPP ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo hadi Juni mwaka 2026, jumla ya mikataba tisa ya PPP imesainiwa kutoka sekta mbalimbali za maendeleo.

‘’Miradi iliyosainiwa ni Mabasi yaendayo Haraka Dar Es Salaam (DART), awamu ya kwanza na ya pili yenye mikataba minne, ikiwemo Mradi wa Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vya Moto na Mradi wa Ujenzi na Uendeshaji wa Jengo la Biashara Kariakoo (DDC)’’, alisema Bw. Taratibu.

Alieleza kuwa, miradi mingine ni pamoja na Ukarabati na Uendeshaji wa Reli Ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na Uboreshaji Bandari ya Dar Es Salaam kupitia kampuni za DP World na ADAN.

Aliongeza kuwa, utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa njia ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), una tija kubwa ndio maana Serikali imeona umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi kama ilivyopewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

‘’PPP ina faida nyingi sana ikiwemo kupata mtaji kutoka Sekta Binafsi na hivyo kupunguza utegemezi wa Bajeti ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo, kupata ujuzi, utaalamu na teknolojia kutoka Sekta Binafsi, kuwezesha upatikanaji wa ajira na mapato kwa Serikali, kuboresha upatikanaji wa huduma kwa ufanisi na kwa wakati pamoja na mgawanyo wa vihatarishi ambavyo kwa kiasi kikubwa vinabebwa na Sekta Binafsi’’ aliongeza Bw. Taratibu.

Alibainisha kuwa mbali na miradi hiyo tisa bado kuna miradi mingine ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na Serikali inafikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, ni maonesho ya 50 toka kuanza kwake ambapo yanaambatana na kuadhimisha miaka 50 ya maonesho hayo.

Hakuna maoni: