Breaking


Jumatano, 15 Julai 2026

TPSF NA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA WAWEZESHA WAFANYABIASHARA KUNUFAIKA NA MASOKO YA AFCFTA, EAC NA SADC

 

Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, limezindua mafunzo maalum ya uhamasishaji kuhusu fursa za biashara katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuongeza ushiriki wao katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristedes Mbwasi, alisema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania wanatumia kikamilifu fursa zinazotolewa na EAC, SADC na AfCFTA, sambamba na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imeitambua sekta binafsi kuwa injini kuu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Katika mafunzo hayo, imeelezwa kuwa AfCFTA inaunganisha soko la zaidi ya watu bilioni *1.4**, huku EAC, SADC na AfCFTA kwa pamoja zikifungua fursa za kufikia soko lenye zaidi ya watu bilioni **1.5** na Pato la Taifa la pamoja linalozidi dola za Marekani trilioni *4**. Aidha, biashara ya ndani ya EAC iliongezeka kwa asilimia 24.5* na kufikia dola bilioni *4.6* katika robo ya pili ya mwaka 2025, huku mauzo ya nje ya Tanzania kwenda nchi za SADC yakiongezeka kutoka dola bilioni *1.3* mwaka 2021 hadi takriban dola bilioni *2.97* mwaka 2024.

Serikali pia ilibainisha kuwa zaidi ya kampuni *49* za Tanzania tayari zimefanikiwa kuuza bidhaa katika masoko ya AfCFTA kwa kutumia Cheti cha Uasili wa Bidhaa (AfCFTA Certificate of Origin), huku bidhaa kama mkonge na bidhaa zake zikipata masoko katika nchi za Ghana, Nigeria na maeneo mengine ya Afrika Magharibi.

Kwa upande wake, TPSF ilieleza kuwa licha ya mafanikio hayo, biashara ya ndani ya Afrika bado inachangia chini ya asilimia *15* ya biashara yote ya bara hilo, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza uelewa wa wafanyabiashara kuhusu fursa zilizopo pamoja na kuwajengea uwezo wa kutumia kikamilifu mikataba ya biashara ya kikanda na bara.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanajengewa uwezo kuhusu matumizi ya upendeleo wa ushuru wa forodha, Kanuni za Asili ya Bidhaa (Rules of Origin), taratibu za kuuza bidhaa nje ya nchi, mahitaji ya viwango na ubora, pamoja na namna ya kutambua na kushughulikia vikwazo visivyo vya ushuru vinavyoweza kuathiri biashara zao.

TPSF imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kujenga uwezo wa sekta binafsi, kuimarisha ushindani wa biashara za Tanzania na kuhakikisha wafanyabiashara wengi zaidi wanatumia kikamilifu fursa zinazotolewa na EAC, SADC na AfCFTA ili kuongeza mauzo ya nje, uwekezaji, ajira na mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Hakuna maoni: