Breaking


Jumatano, 8 Julai 2026

WMA YATUMIA MAONESHO YA SABASABA KUHAMASISHA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI


Dar es Salaam, Julai 8, 2026 – 


Wakala wa Vipimo (WMA) unaendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika biashara na kulinda haki za walaji pamoja na wafanyabiashara.

Katika siku ya 11 ya maonesho hayo, viongozi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali wameendelea kutembelea banda la WMA kwa lengo la kujifunza huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, ikiwemo usahihi wa vipimo vinavyotumika katika shughuli za biashara.

Mbali na kutoa elimu, WMA imekuwa ikigawa zawadi mbalimbali zenye nembo na ujumbe wa kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi kwa wadau wanaotembelea banda hilo, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa wa umma kuhusu jukumu la wakala huo.

Aidha, wageni wanaotembelea banda la WMA wanapata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu kuhusu masuala mbalimbali ya vipimo vinavyotumika katika biashara za kila siku, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha vinazingatia viwango vinavyotakiwa.

WMA imewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda lake ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zake na umuhimu wa kutumia vipimo sahihi kwa maendeleo ya biashara yenye haki, uwazi na uaminifu.


Hakuna maoni: