Madrid, Hispania
Klabu ya Atlético Madrid imesema haitafanya mazungumzo na FC Barcelona kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wake, Julián Álvarez, baada ya uamuzi huo kuungwa mkono kwa pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo.
Kupitia taarifa rasmi, Atlético Madrid imesema Bodi ya Wakurugenzi imeunga mkono kwa kauli moja msimamo wa klabu wa kutofanya mazungumzo na Barcelona kuhusu uhamisho wa Álvarez.
Klabu hiyo imeeleza kuwa iko tayari kushiriki mazungumzo ya uhamisho katika mazingira ya maadili, weledi na heshima kati ya klabu. Hata hivyo, imedai kuwa Barcelona haijakidhi masharti hayo katika suala la Álvarez.
“FC Barcelona haijakidhi mahitaji hayo na, kutokana na hilo, hakujakuwa na mazungumzo, wala hakutakuwa na mazungumzo nao kuhusu Álvarez,” sehemu ya taarifa ya Atlético Madrid imeeleza.
Atlético pia imesema inaamini Álvarez ataelewa uamuzi huo na kuendelea kuelekeza nguvu zake katika kuisaidia klabu kufikia malengo yake, kama alivyofanya katika misimu miwili ambayo ameitumikia klabu hiyo.
Álvarez alijiunga na Atlético Madrid akitokea Manchester City na amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha klabu hiyo. Kauli hii ya Atlético inaweka wazi msimamo wake kuhusu uwezekano wa mshambuliaji huyo kuhamia Barcelona.
Kwa sasa, Atlético Madrid imesisitiza kuwa hakuna mazungumzo na Barcelona kuhusu uhamisho wa Julián Álvarez na haitarajii kuanzisha mazungumzo hayo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni