Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Othman Yakubu, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi zake za kuhifadhi maeneo ya Urithi wa Dunia na kuyatumia kuchochea maendeleo ya utalii nchini.
Mhe. Balozi Yakubu ametoa pongezi hizo leo, Agosti 31, 2026, alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, na kumpa taarifa kuhusu ziara yake ya kikazi katika maeneo mbalimbali ya Urithi wa Dunia na vivutio muhimu vya utalii nchini.
Ziara hiyo, iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kufanyika kuanzia Agosti 14 hadi 28, 2026, ilimfikisha Balozi Yakubu katika maeneo mbalimbali ya Urithi wa Dunia na vivutio vya utalii, ikiwemo Kondoa, Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro, Kilwa, Zanzibar na Selous, ambapo alifanya mikutano na mazungumzo na wadau wa uhifadhi na utalii.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Yakubu alisema ziara hiyo imemwezesha kujionea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utunzaji wa urithi wa asili na utamaduni, uboreshaji wa miundombinu ya utalii na juhudi za Serikali za kuongeza thamani ya maeneo hayo kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.
“Nimejionea kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake katika kulinda maeneo yetu ya Urithi wa Dunia na kukuza utalii. Maeneo haya si fahari ya Tanzania pekee, bali ni rasilimali muhimu inayoweza kuendelea kuvutia watalii na uwekezaji, kuongeza ajira na kukuza mapato ya Taifa,” alisema Mhe. Balozi Yakubu.
Aidha, Balozi Yakubu amesema uzoefu alioupata utasaidia kuimarisha uwakilishi wa Tanzania ndani ya UNESCO, hasa katika masuala ya uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya maeneo ya Urithi wa Dunia.
Kwa upande wake, Dkt. Abbasi amempongeza Balozi Yakubu kwa ziara hiyo na juhudi zake za kuitangaza Tanzania kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara, Uwakilishi wa Tanzania katika UNESCO na taasisi nyingine za uhifadhi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni