Uamuzi huo umeanza kutumika katika udahili wa mwaka wa masomo 2026/27, baada ya Bodi ya Usimamizi wa Mfuko huo kuridhia kutumia mifumo ya HESLB katika mchakato wa kutangaza, kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi wanaostahili kupata ufadhili.
Akizungumza leo, Agosti 28, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mwongozo Mpya wa Utoaji Ufadhili kwa Wanafunzi wanaonufaika na Mfuko huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema hatua hiyo inalenga kuboresha namna wanafunzi wanavyopatikana na kunufaika na ufadhili.
Gavana Tutuba amesema tangu mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 2009, nafasi za ufadhili zilitangazwa kupitia vyombo vya habari, ikiwemo televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii. Wanafunzi wenye sifa waliwasilisha maombi yao, ambayo yalichambuliwa na timu ya wataalamu kutoka BoT.
Amesema mabadiliko hayo yanaendana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza nafasi na kusubiri wanafunzi kuwasilisha maombi, HESLB itaweza kutumia mifumo yake iliyopo kuchakata taarifa za wanafunzi na kubaini wale wanaokidhi vigezo vya kupata ufadhili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema jukumu hilo ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo na ni ishara ya imani iliyowekwa na BoT katika uwezo wa HESLB kusimamia mchakato wa utoaji wa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi.
Dkt. Kiwia amesema HESLB imewekeza zaidi ya dola milioni tano katika kujenga na kuimarisha mifumo yake ya kidijitali inayowezesha usimamizi wa mchakato mzima wa mikopo na ufadhili wa wanafunzi.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni