Breaking


Jumatano, 19 Agosti 2026

BRELA NA MAAFISA BIASHARA KUSHIRIKIANA KUTEKELEZA DIRA 2050

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amewaelekeza Maafisa Biashara nchini kushirikiana kwa karibu na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo, ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ili kutekeleza kikamilifu Dira 2050.

Naibu Waziri Londo ametoa maelekezo hayo  alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara,  Judith Kapinga, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tatu cha Wizara na Maafisa Biashara Nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi, Londo alieleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini hivyo ni muhimu kushirikiana.

Aliongeza kuwa Dira 2050 inataka sekta ya umma kutoka kuwa mdhibiti wa biashara kwenda kuwa mwezeshaji wa Viwanda, biashara na uwekezaji. Hivyo, Maafisa Biashara mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutambua na kuondoa urasimu usio wa lazima, kutoa taarifa sahihi, kurahisisha upatikanaji wa leseni, kusaidia urasimishaji wa biashara na kuhakikisha wafanyabiashara hawapotezi muda kwa kuzunguka katika ofisi nyingi kupata huduma.

Hakuna maoni: