Breaking


Alhamisi, 20 Agosti 2026

ELIMU YA MABADILIKO YA SHERIA ZA KODI YAWAFIKIA WAFANYABIASHARA WA KARAGWE

Wafanyabiashara wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wamepatiwa elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2026/27, katika semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano.

Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa ELCT Kayanga, mjini Kayanga ambapo maafisa wa TRA wamewapatia wafanyabiashara uelewa kuhusu mabadiliko mbalimbali ya sheria za kodi pamoja na namna yanavyogusa shughuli zao za biashara.

Elimu hiyo hutolewa na TRA kila mwaka kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuelewa mabadiliko ya sheria za kodi, kutambua haki na wajibu wao wa kikodi, na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

Aidha, elimu hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara kutambua fursa mbalimbali za kibiashara zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya sheria na taratibu za kodi, pamoja na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kikodi kwa usahihi.

Katika semina hiyo, maafisa wa TRA pia wamewasisitiza wafanyabiashara umuhimu wa kutunza kumbukumbu sahihi za biashara zao, ikiwa ni pamoja na kutoa na kudai risiti halali za EFD/VFD kila wanapofanya mauzo au manunuzi.


TRA imeendelea kutoa elimu kwa walipa kodi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa masuala ya kodi, kuimarisha ulipaji kodi wa hiari na kujenga mazingira bora ya kufanya biashara nchini.

Hakuna maoni: