Breaking


Jumamosi, 1 Agosti 2026

KAMISHNA WA IDARA YA UPELELEZI WA KODI AKUTANA NA MKUU WA WILAYA YA KINONDONI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA MAGENDO


Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Hashim Ngoda, amekutana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambule, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya magendo katika maeneo ya Kunduchi, Mbweni na Bagamoyo. Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TRA, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na vyombo vingine vya dola ili kuziba mianya ya magendo, kulinda mapato ya Serikali na kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa.


Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mtambule amesema kuanzia Daraja la Tanzanite mpaka Bagamoyo, Pangani ni  miongoni mwa maeneo yanayotumiwa kupitisha bidhaa kwa njia zisizo halali, hususan mafuta ya kula kutoka Zanzibar yanayoingia nchini bila kufuata taratibu za kisheria. Ameeleza kuwa bidhaa zinazoingizwa kwa njia hizo ni vigumu kuthibitisha ubora na usalama wake kwa matumizi ya binadamu, hivyo tayari wameunda kikosi kazi na wataendelea kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, maafisa wa Serikali pamoja na wananchi wa Bagamoyo na maeneo jirani ili kuimarisha mapambano dhidi ya magendo.


Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Kodi, Bw. Hashim Ngoda, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa ushirikiano na utayari wake wa kuunga mkono juhudi za TRA katika kupambana na magendo. Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali na wananchi utasaidia kuongeza ufanisi katika kudhibiti uhalifu wa kimagendo, kulinda afya za wananchi na kuhakikisha Serikali inaendelea kukusanya mapato stahiki kwa maendeleo ya Taifa.

Hakuna maoni: