Breaking


Alhamisi, 27 Agosti 2026

MALARIA YAUA WAFANYAKAZI WAWILI WA UWANJA WA NDEGE WA FRANKFURT



Wafanyakazi wawili wa Uwanja wa Ndege wa Frankfurt nchini Ujerumani, wamefariki dunia kutokana na malaria, baada ya mlipuko nadra wa ugonjwa huo kusababisha wafanyakazi sita kuambukizwa ugonjwa huo hatari unaoenezwa na Mbu.

Inaaminika kuwa Mbu hao waliwasili katika uwanja huo, ambao ni mkubwa zaidi nchini Ujerumani, wakiwa ndani ya ndege. 

Kwa mujibu wa mamlaka za afya ya umma nchini humo, mlipuko huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Julai mwaka huu.

Msemaji wa kampuni ya Fraport, inayosimamia Uwanja wa Ndege wa Frankfurt, amesema mfanyakazi mmoja amefariki kutokana na maambukizi hayo. 

Hata hivyo, baadaye mamlaka za afya ya umma zilitangaza kuwa watu wawili kati ya sita walioathirika wamefariki dunia.

Tayari, mitego maalumu ya kunasa mbu imewekwa katika uwanja huo, huku mbu watakaonaswa wakipelekwa maabara kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini aina yao na walikotoka.

Hakuna maoni: