Breaking


Jumamosi, 29 Agosti 2026

MAWAKILI WA SERIKALI MKOA WA MWANZA WAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJI WA DIRA 2050



Mawakili wa Serikali wapatao 112 kutoka Taasisi za Serikali 33 wameshiriki katika Mkutano maalum wa Mawakili wa Serikali ulioandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Mkoa Mwanza na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Rock City Mall jijini Mwanza tarehe 28 Agosti,2026.


Akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, aliwasisitiza Mawakili wa Serikali kutumia vyema nafasi yao, Wajibu na Majukumu yao ili kuweza kuyafikia malengo ya Dira 2050.


Aidha, Mhe. Makilagi aliipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa Mkutano huo muhimu, kwa Mawakili wa Serikali.


Akitoa salamu kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Ilemela, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Kafiti William Kafiti aliwasisitiza Mawakili wa Serikali kusimama katika weledi na taaluma yao ili kuishauri vizuri Serikali na kuwezesha mafanikio ya Taifa letu. 


Awali, akimkaribisha mgeni rasmi na kueleza lengo la Mkutano huo Wakili wa Serikali Mkoa wa Mwanza Bw. Kabyemela Lushagara alieleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliona kuna umuhimu kwa Mawakili wa Serikali Mkoa wa Mwanza kukutana ili kueleweshana, kufahamishana juu ya nafasi yao katika utekelezaji wa Dira,2050. 


Bw.Lushagara alieleza kuwa Mawakili wa Serikali ndio "guardians" wa Regulatory regime na Legal Frameworks za Nchi yetu hivyo ni muhimu waifahamu Dira vizuri na pia wawe na maarifa ya kisasa na weledi ambao unanyumbulika na nguvu ya kiuchumi, soko, biashara, TEHAMA na mambo ya kijiopolitiki kwasababu ni nguzo muhimu katika utekekezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Vilevile, Bw. Lushagala alilisisitiza umuhimu wa Mawakili kupewa nafasi stahiki katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika taasisi zao hasa katika eneo la uingiaji na usimamizi wa mikataba ili kuwezesha kupata "value for money" kwa fedha za Serikali na za Wawekezaji. 


Mawakili wa Serikali wa Mkoa wa Mwanza katika Mkutano huo waliazimia kuanzisha jukwaa  rasmi la Mwakili wote wa Serikali wa Mkoa wa Mwanza litakalo wawezesha kukutana na kubadilishana uzoefu.

Hakuna maoni: