Breaking


Jumapili, 30 Agosti 2026

MNH-MLOGANZILA YAFANYA UPANDIKIZAJI WA MENO KWA MARA YA KWANZA KUPITIA MADAKTARI WAZAWA



Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeanza rasmi kutoa huduma ya upandikizaji wa meno kupitia madaktari bingwa wazawa, hatua inayolenga kuongeza wigo wa huduma za kibingwa za matibabu na upandikizaji wa meno nchini.


Tangu mwaka 2024, hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma hiyo kupitia kambi maalum kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka India, hatua iliyowawezesha madaktari bingwa wazawa kupata uzoefu na kujengewa uwezo katika kutoa huduma hiyo.


Baada ya kujengewa uwezo, wataalamu hao wameanza kutoa huduma ya upandikizaji wa meno bila kutegemea kambi maalum, ambapo huduma hiyo itatolewa kila wiki ya kwanza ya kila mwezi, hatua itawawezesha wananchi kupata huduma hiyo ya kibingwa kwa urahisi zaidi ndani ya nchi.


Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso, Mataya, Kinywa na Meno, Dkt. Dominicus Kabogo, amesema upandikizaji wa meno hufanyika kwa mtu aliyepoteza jino kutokana na kung’olewa au ajali, ambapo kifaa maalum kinachoitwa implant hupandikizwa kwenye mfupa wa taya katika eneo ambalo jino limepotea.


Dkt. Kabogo amesema huduma hiyo humsaidia mgonjwa kurejesha mwonekano na utendaji wa meno kwa hali inayokaribiana na meno ya kawaida, huku ikipunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya meno bandia yanayohitaji kuvuliwa na kuvaliwa mara kwa mara.


Hakuna maoni: