Breaking


Jumamosi, 1 Agosti 2026

MYKHAYLO MUDRYK AVUNJA UKIMYA BAADA YA KURUHUSIWA KUREJEA UWANJANI

Mchezaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Ukraine, Mykhaylo Mudryk, ametoa kauli yake ya kwanza baada ya kuthibitishwa kuwa yuko huru kurejea kucheza soka kufuatia kuondolewa kwa marufuku aliyokuwa amewekewa.

Kupitia taarifa yake, Mudryk amesema anafurahia kuona mchakato wa kesi yake umefikia tamati na kwamba sasa anaweza kuendelea na maisha yake ya soka.

“Baada ya mchakato mrefu, marufuku ya miaka minne niliyowekewa imefutwa na sasa niko huru kuendelea na kazi yangu mara moja.”

Mshambuliaji huyo amesema kipindi hicho kilikuwa kigumu zaidi katika maisha yake ya soka, lakini hakuwahi kupoteza matumaini ya kuthibitisha msimamo wake.

“Tangu mwanzo wa kesi hii nilisisitiza kuwa sikuwahi kutumia, kwa kujua au kwa makusudi, kitu chochote kilichopigwa marufuku. Dhamira yangu imekuwa kushindana kwa haki na kuiwakilisha klabu pamoja na nchi yangu kwa uadilifu.”

Mudryk pia ametoa shukrani kwa familia yake, marafiki, wachezaji wenzake, viongozi wa Chelsea FC, mashabiki wa klabu hiyo na timu yake ya wanasheria kwa msaada waliompa katika kipindi chote cha kesi.

Amesema sasa analenga kurejea uwanjani, kufanya kazi kwa bidii na kutoa mchango chanya kwa klabu na timu yake.

Akihitimisha ujumbe wake, Mudryk aliwashukuru wote walioendelea kumuamini na kueleza kuwa ana matumaini makubwa kuhusu hatua inayofuata katika maisha yake ya soka.


Hakuna maoni: