Dodoma:
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Bunge la 13, Mkutano wa Nne, limeahirishwa hadi Jumanne, Oktoba 27, 2026, huku akitoa maelekezo mbalimbali yanayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, Dkt. Nchemba amezielekeza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa ya Mwendokasi (SGR).
Dkt. Nchemba amesema kukamilika kwa mtandao huo wa reli pia kutawezesha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma kuunganishwa na huduma ya SGR kupitia Tabora, na hivyo kurahisisha usafiri kuelekea Dodoma na Dar es Salaam.
Katika sekta ya madini, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa leseni za madini ambazo hazijaendelezwa zifutwe kwa mujibu wa sheria, huku maeneo hayo yakigawiwa upya kwa vijana na wachimbaji wadogo wa Kitanzania.
Aidha, amezitaka taasisi za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali hizo katika maeneo yenye vipaumbele vya maendeleo.
Pia, amewahamasisha Watanzania wenye uwezo kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga mfumo imara wa afya utakaowezesha pia wananchi wasio na uwezo kupata huduma bora za afya.
Vilevile, Dkt. Nchemba amewasisitiza watendaji wa Serikali kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zao kwa wakati na kutoa mrejesho unaostahili, bila kusubiri ziara za viongozi wakuu.
Amesema kuna wajibu wa kuhakikisha kuwa mipango, sera na maamuzi ya Serikali yanazaa matokeo yanayogusa na kuboresha maisha ya wananchi kwa vitendo.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni