Breaking


Jumanne, 8 Septemba 2026

KAMATI ZA USHAURI WA KISHERIA ZAZINDULIWA KATAVI, WANANCHI WAPATIWA HUDUMA ZA SHERIA BILA MALIPO



Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, imezindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya katika Mkoa wa Katavi. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 8 Septemba, 2026 na kufuatiwa na kliniki ya Sheria bila malipo iliyoanza tarehe 7 Septemba, 2026 katika Viwanja vya Azimio Mpanda .


Uzinduzi wa Kamati za Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Kisheria bila malipo, ni  dhamira ya dhati ya Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kutatua migogoro, kutoa ushauri wa Kisheria kwa wananchi na elimu ya Kisheria bila malipo.


Akizungumza katika hotuba yake ya Uzinduzi, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Jamila Yusuph, ameeleza  kuwa jukumu la kutatua migogoro katika maisha ya watanzania sio la Serikali pekee ni jukumu la wadau wote wa maendeleo.


Mhe. Mkuu wa Wilaya amekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko katika Uzinduzi wa Kamati za Kudumu za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya zimezinduliwa mkoani Katavi, tarehe 8 Septemba , 2026, katika Viwanja vya Azimio, Mpanda.


Akizungumza katika hafla hiyo,  amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kamati hizo pamoja na Kliniki ya Sheria ili kupata elimu, ushauri na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria.


Akitoa shukrani zake  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari, amesema kuwa kitendo  cha kusogeza huduma ya ushauri wa kisheria kwa wananchi wa mkoa wa Katavi zinaenda kutatua changamoto walizonazo wananchi za kisheria.


*“Namshukuru Mhe. Hamza Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi yake na Kamati ya kudumu ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Ofisi yangu, kuweza kufanikisha sherehe hii ya Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria bila Malipo Mkoa wa Katavi.”* Amesema  Mhe. Jamila Yusuph.


Amesema uwepo wa Kamati za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya utasaidia kuimarisha uratibu wa huduma za kisheria na kuhakikisha wananchi wanapata kufahamu wajibu wao pamoja na taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali.


Amewataka wananchi wa Katavi na maeneo jirani kutumia kikamilifu fursa ya Kliniki ya Sheria inayotolewa bila malipo, hususan kwa wananchi wenye uhitaji wa elimu na ushauri wa kisheria.


Awali akimkaribisha mgeni rasmi Bw. Nehemia James, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Katavi, akimuwakilisha  Katibu tawala wa Mkoa wa Mkoa wa in Katavi  ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa  kusogeza huduma ya ushauri wa kisheria kwa Wananchi wa mkoa wa Katavi.


*“Tunashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta kliniki ya sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi bila shaka,ni manufaa kwa wananchi wa mkoa wetu.”* Amesema Bw. Nehemia


Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa huduma za kisheria Mkoa wa Katavi umefanyika rasmi tarehe 8 Septemba, 2026,  Huku Kliniki ya Sheria bila malipo ikiendelea katika Viwanja vya Azimio, Mpanda, ambapo wananchi wanapata huduma za ushauri wa kisheria bila malipo kuanzia tarehe 7 Septemba, 2026 hadi tarehe 13 Septemba, 2026.

Hakuna maoni: