Breaking


Ijumaa, 25 Septemba 2026

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA UONGOZAJI NDEGE ILI KUIMARISHA USALAMA



Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), inaendelea kuimarisha huduma za uongozaji ndege katika viwanja vya ndege vya Mikumi, Kogatende na Seronera vinavyoendeshwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza usalama na ufanisi wa usafiri wa anga nchini.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Kamati ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga (NCASC), iliyoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri K. Bakari, katika viwanja hivyo Septemba 24, 2026.

Katika ziara hiyo, Kamati imejionea uwepo wa mitambo ya kisasa ya hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automated Weather Stations – AWS) katika viwanja vyote vitatu vya Mikumi, Kogatende na Seronera. Mitambo hiyo inawezesha upatikanaji wa taarifa muhimu za hali ya hewa zinazosaidia uendeshaji salama na wenye ufanisi wa ndege.

Katika Kiwanja cha Ndege cha Mikumi, Kamati imejionea runway mpya yenye urefu wa kilomita 1.8, ambayo ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika kuimarisha miundombinu inayowezesha shughuli za usafiri wa anga kufanyika kwa usalama na ufanisi zaidi.

Aidha, katika Kiwanja cha Ndege cha Seronera, Kamati imekagua maendeleo ya ujenzi wa Mnara wa Uongozaji Ndege (Control Tower), ambao utakapokamilika utaimarisha zaidi uratibu na usimamizi wa shughuli za ndege katika kiwanja hicho.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Bakari amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha huduma za uongozaji ndege na miundombinu inayosaidia shughuli za anga nchini.

“Uwekezaji unaoendelea kufanyika katika huduma za uongozaji ndege, mitambo ya kisasa ya hali ya hewa na miundombinu ya viwanja vya ndege ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama na ufanisi wa usafiri wa anga nchini. Hatua hizi pia zinaongeza uwezo wa viwanja vinavyohudumia maeneo ya hifadhi na kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii,” amesema Dkt. Bakari.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa huduma hizo katika viwanja vinavyohudumia maeneo ya hifadhi kunarahisisha ufikaji katika vivutio vya utalii na kuongeza mchango wa usafiri wa anga katika maendeleo ya utalii na uchumi wa Taifa. 



Hakuna maoni: